Taifa halina nguo, nani atalivisha?
Na Deus Bugaywa
Bwana Yesu akiwa katika kilele cha mateso yake huku amelemewa na msalaba mzito, kuelekea Golgotha ambako alisuribiwa, akina mama wa Israel walikuwa wanabubujikwa machozi kumlilia kwa huruma ya mateso makali aliyokuwa akipata.
Lakini Mwenyewe aliwaambia kwamba hawana haja wala sababu ya kumlilia yeye, isipokuwa wajililie wao na nafsini zao n watesi wake kwa sababu ya dhambi zao na kwa kuwa upanga tayari uko juu yao.
Hatuwezi kubishana sasa hivi juu ya nchi yetu kuyumba, hilo ni jambo ambalo kila mwenye macho ya kuonana akili ya kufahamu analiona. Walau Kongamano la maadhimisho ya miaka kumi tangu kifo cha baba wa taifa limetufungua na kutambua kumbe mgogoro wetu uko wapi.
Na hivyo tunajua kwamba tangu mwaka 1995 nchi hii ingeweze kwenda segemnege kama inavyokwenda sasa kama isingekuwa kwa hekima na busara na kuogopwa na kuheshimiwa kinafiki kwa mwalimu Nyerere na wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM.
Nasema walimheshimu kinafiki kwa sababu walilazimika tu kukubaliana naye siyo kwa sababu walielewa na kuona mantiki ya hoja zake, lakini kwa kuwa walikuwa wanajua hawawezi kumudu kutofautiana na mzee huyo.
Kwa hiyo wakati dunia inaomboleza kifo cha mwana shujaa huyu wa Afrika wapo wanafiki wakubwa miongoni mwetu ambao walishusha pumzi za ahueni, kuashiria kikwazo kikubwa kilichokuwa mbele ya kufikia malengo yao ya ubinafsi na kuifanya Tanzania kama mali yao sasa hakipo tena. Na hiyo ndiyo hali tunayoiona sasa, hakuna mtu anaweza kumkemea mtu kufanya lolote lile kwa sababu zozote zile, taifa linakwenda kiholelaholela tu.
Pengine baada ya miaka kumi ya Tanzania bila baba wa Taifa tuna hoja za kujiuliza kama tunapaswa tuendelee tu kumlilia na kutamani kama angekuwa bado yuko hai kitu hiki au kile kisingefanyika au tuanze kujililia sisi wenyewe na nafsi zetu na kwa kweli kuchukua hatua za kuyaishi yale ambayo tunaamini kwamba ndiyo ulikuwa msingi wa Tanzania moja yenye haki na usawa?
Ni kweli kwamba sasa hivi katika CCM hayupo mtu anayeweza kuuliza maswali matatu, kama ambayo Mzee Butiku ametueleza, yale aliyoyauliza Mwalimu wakati wa mkutano Mkuu ule wa mwaka 1995.
Nani atawauliza viongozi wetu wa leo kama wao ni wahuni au viongozi? Na pili, kwa zogo na vurugu zile ndiyo staili ya kuchagua Rais? Na hili la tatu ndio la muhimu sana kwetu kwamba, Je Watanzania kama wangewaona, je wangeamini kuwa ninyi ni viongozi wao?
Walau jambo moja linajidhihirisha kwetu hapa ni kwamba wajumbe wanaokutana katika mkutano wa kuchagua mtu ambaye anatarajiwa kuwa Rais wa nchi hii, huwa wana mabo ya jabu ambayo Mwalimu hakusita kuwahoji tofauti ya mkusanyiko huo wa kuchagua rais na wahuni, hata yeye alifika mahali kashindwa kutambua hawa waliokutana humo ni viongozi au wahuni? Sina hakika walijibu nini.
Watanzania walau sasa tumeshaona na tunajua madudu mengi na jinsi viongozi wetu wanavyofanya, hivi bado tunaamini kuwa hao ni viongozi wetu? Mwalimu aliwashangaa na viongozi wale kwa kuwa alijua salama yao mbele ya Watanzania ni kwa vile walikuwa hajaona wanavyofanya mambo ambayo unaweza kuyaita ya kitoto wakati wana dhamana ya kuongoza nchi, na akajua laiti Watanzania wakijua bila shaka hawa wasingestahili kuwa viongozi, kwa sababu Watanzania wasingeamini kuwa hao ni viongozi wao.
Lakini ndio tulio nao, na ndio hao tunawashuhudia wakipashana na kuvuana nguo hadharani kweupe, kwenye majukwaa rasmi na kulumbana kwa maslahi yao binafsi kuliko ya kwa ajili ya mustakabali wa taifa, bado tunaamini hawa ni viongozi wetu?
Bila shaka ili kuisaidia nchi hii ni lazima kama hayupo mtu ambaye anaweza kuwauliza maswali hayo na wakamsikiliza na kumheshimu hata kama ni kwa unafiki tu, jukumu hilo linatuanguakia sisi wananchi moja kwa moja.
Kwa sababu hatimaye sisi ndio tunaolipa kila gharama ya madudu haya yanayofanywa na viongozi ambao wanajiita wanatokana na sisi hata kama wanayofanya na kutenda hayana maslahi kwetu kama taifa.
Ni lazima tufike mahali tuache kunung’unika na kulaumu kwa chini chini, tuchukue hatua za kuacha unafiki ili tuweze kulikoa taifa letu na hatari kubwa inayolikabili mbele yake kama tukiendelea na unafiki huu tunaokwenda nao kwa sasa.
Hata makada wa chama wanaojiita kwamba wako upande wa wananchi waoneshe hivyo kweli siyo kwa mashaka mashaka, kama kweli wameamua kupambana kwa ajili ya wananchi na kwa maslahi ya Tanzania hawana haja kung’ang’ania kujinasabisha na watu ambao wanaamini kuwa wako kinyume chao.
Giza na nuru haviwezi kukaa pamoja hata kwa bahati mbaya, kimoja kikiwepo lazima kingine kikimbie, kama kwa mfano ndani ya CCM wako watu ambao wanatuhumiwa ni mafisadi na ambao ndiyo wanaiyumbisha nchi hii, na kuna wengine ambao wanaamini ni wasafi, hakuna namna hawa wanaweza kukaa pamoja, mwanga hata uwe hafifu namna gani ukiumulika kwenye giza utajipambanua tu.
Tunaambiwa Mwalimu katika mkutano mkuu ule aliwambia wajumbe kama wataendelea na msimamo wao wa utovu wa nidhamu na kushabikia mgombea aliyewahonga, basi waende kwa wananchi, wao wapite huku na wengine wapite kule waone wananchi wataamua nini.
Kama CCM inahitaji kuendelea kuwepo apatikane mtu wa aina hiyo, lakini bahati mbaya kubwa kwao ni kwamba hawana mtu wa aina hiyo, kila anayetaka kuwaeleza na kuwasaidia wauone ukweli wanakurupuka na visingizio vya kitoto kwamba anayesema anatafuta umaarufu au ana wivu kwa kuwa alishindwa katika uchaguzi au hakuwa mwanamtandao.
Ndio maana nasema kutokuwepo kwa nabii au mtume hakuna maana kwamba mafundisho yake hayapo, kawaida manabii wanakuja na kuacha ujumbe ambao unatarajiwa uwaongoze wafuasi kwa muda wote ambao nabii hatakuwepo.
Ni kweli baba wa taifa hatuko nae lakini sisi ambao tunaamini hekima zake zina umuhimu wa pekee kwa ajili ya kuijenga Tanzania yenye amani na usawa hatuna hiari ila kuvaa viatu vyake na kuanza kuisimamia misimamo yake.
Tumeambiwa nchi inatembea uchi, na ni kweli ukiangalia unaona kabisa hakuna hata rapa la nguo la kuistili, watu pekee wenye kumudu kuistili ni sisi ambao tunaona na kukubali ukweli kwamba taifa liko utupu.
Hatuwezi kuwategemea wale waliolivua nguo taifa hili walivishe, kwa sababu hawafanyi hivyo kwa bahati mbaya, wanalivua nguo taifa makusudi kwa malengo maalum, na siyo kwamba hawajui kuwa liko utupu la hasha, tofauti yetu na wao ni kwamba wakati sisi tunakiri hivyo wao hawataki kukiri ukweli huo.
Ni wajibu wetu bila kujali itikadi zetu, wajibu huu unatuangukia sisi kama Watanzania siyo kwa sababu nyingine yeyote ile, na kwa hili hakuna mwenye hisa zaidi ya mwingine, hatujachelewa kiasi hicho kama tukimua sasa kuuvua unafiki bado tuna muda tunaweza kulikoa taifa hili.
Mungu ibariki Tanzania.
0754 449 421, drbugaywa@yahoo.com
Tuesday, December 22, 2009
Subscribe to:
Posts (Atom)