Friday, February 19, 2010

Kamata! Shika! na mwenyewe nyuma…..!

Na Deus Bugaywa

Ukiwaangalia Watanzania wa leo utaona kwenye fikra zao, nyuso zao na hisia zao utaona wazi kabisa kuwa iko kiu ya mabdiliko. Watu wanataka mabadiliko wamechoka na mazoea waliokuwa nayo na ambayo yanaendelea kuwafanya wawe dhalili.
Kila mtu anatamani mambo yaache kuwa na hali ilivyo sasa, anatamani yachukue mkondo mpya na njia mbadala ambayo inaweza kuwa na matumaini. Katika hali hii unatarajia kuwa wao ndiyo wawe chemichemi na chachu ya mbadiliko.
Bahati mbaya kwetu ni kwamba, tunataka na kutamani mabadiliko lakini hatuko tayari kulipa gharama za mabadiliko hayo. Tunataka matokeo yaje tu kutoka hewani bila sisi kuhusika kwa namna yeyote ile kuyasababisha.
Katika hili tunapaswa kujifunza kwa ujumbe wa mabadiliko wa Rais wa Marekani Barack Obama kwamba “The change we seek will not come easy, that it will not come without its share of sacrifice and struggle”, kwamba mabadiliko tunayoyataka hayawezi kuja kirahisi na hayawezi kuja bila juhudi na kujitolea.
Majitoleo yanayozungimziwa hapa ni pamoja na kukubali kuachana na mazoea mabaya ambayo tunayaona kuwa kama sehemu ya maisha yetu, kwamba hata kama tunaumizwa sana na mazoea hayo, hatuko tayari kuyavua na kuvumilia uchungu kidogo wa muda ili tupate nafanikio ya muda mrefu.
Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi ambao Watanzania tunatakiwa kutumia haki yetu ya kikatiba kuchagua aina ya viongozi ambao wanaweza kutuletea mabadiliko tunayoyatamani. Tunatakiwa tuutambue ukweli kwamba mambo mazuri ya kimaendeleo tunayoyatamani yana uhusiano wa moja kwa moja na aina ya viongozi tunaowachagua.
Jiulize Mtanzania, wewe mahali ulipo una mwakilishi wako mbunge na diwani, lakini kuna kero nyingi sana mtaani kwako, katani na jimboni kwako, kiongozi huyo anatakiwa kuwa mhamasishaji wa maendeleo katika jimbo na kata yenu.
Yako mambo ambayo hayahitaji hata nguvu ya serikali kuyafanya yawezekane, mambo mengine kama barabara za jimboni kwenu, huduma za maji na vitu vya aina hiyo vinategemea sana aina ya kiongozi wenu, kama ana sifa za kufaa kuwa kiongozi anaweza kabisa kuwahamasisha ninyi wanajimbo na kata na kuishwishi serikali kuweka nguvu kidogo ili kufanikisha maendeleo yenu.
Wako Watanzania leo wana mbunge huyo huyo kwa miaka 15 au zaidi lakini hajawahi kuwa na mchango wa maana kwa katika kuhamasisha maendeleo ya jimbo lake, huyu hata kama ni mjombe wenu, mmezalia kijiji kimoja au ni swahiba wako sana, hafai kuwa mbunge wa jimbo lako.
Kama katika miaka hiyo kwa vipindi vitatu hajafanya mambo ya msingi, anaonekana jimbo mara moja kwa miezi sita, kwa mwaka anaonekana jimboni mara mbili kama sikuku za Eid el fitri na Eid al Haji, huyu hata akipewa miaka 25 mingine hawezi kuleta mabadiliko ya maana jimboni kwako.
Wabunge wa aina hii ni wajanja sana katika kipindi kama hiki anakuwa mnyenyekevu na vizawadi kwa viongozi mbali mbali wa chama na watu wenye ushawishi jimboni ili waweze kurubuni ninyi mliobaki ili mmuone ni aina ya mtu kweli mnayemhitaji.
Huyu katika hali ya kawaida anacheza na akili zenu tena ni kashfa kwenu ninyi kwa kuwa anaowaona kama watoto wadogo mnaoweza kudanganywa na ‘peremende’ mkadanganyika, na anakuwa anawapuuza hivyo hivyo kila mwaka ndiyo maana bado ni mwakilishi wenu kwa miaka yote hiyo.
Wanaharakati wa ukombozi wanamsemo mmoja kuwa “The most potent weapon of the oppressor is the mind of the oppressed”, kwamba silaha muhimu sana kwa wakandamizaji ni akili za waandamizwaji.
Ni kweli wala hatuwezi kubishana katika hili, kwamba viongozi wetu hawa wanaotuongoza wanatunyanyasa na kutumia nafasi za umma tulizowapa dhamana kutuongoza kuelekea kwenye maendeleo yetu kama taifa, wanazitumia kwa manufaa binafsi kwa sababu ya umbumbu wetu.
Mnamwona mbunge wenu yuko ‘bize’ na mambo yake kuliko ya umma ambayo aliomba kuwa mtumishi wenu ili awatumikie, badala yake hata kumona tu mmweleze maoni yenu na jinsi mnavyoona mnaweza kukabiliana na changamoto zenu katika jimbo inakuwa ni kazi ngumu kumuona kama vile unataka kuonana na malkia.
Msomaji mmoja wa Kanda ya Ziwa alieleza masikitioko yake jinsi ambavyo wamefanya juhudi za kutaka kumuona mbunge wao kwa muda wa mwaka mzima lakini hawakufanikiwa badala wanaishiakuelekezwa kuonana na katibu wake.
“Hata tulipompigia simu mara kadhaa, kwa sababu hata jimboni haishi, alituelekeza tuonane ana katibu wake tu, tukaisisitiza katibu anajua na hana msaada akasema akija atatupatia nafasi tumuone, siku amekuja kulikuwa na mafuriko ya watu hatukumuona mpaka tukakata tama, sasa ndugu mwandishi huyu kweli anafaa kuwa kiongozi?”, alihitimisha msomaji wangu kwa kunihoji.
Nilimwelewa mahangaiko aliyokuwa nayo pamoja na wananchi wenzake, lakini nilimjibu nikamwambia, katika kila jamii kuna uwezekano mkubwa wa kupata kiongozi anayewastahili zaidi kuliko mnayemtaka, kwa hiyo kumlaumu Mheshimiwa huyo inaweza kuwa ni kumonea kwa kuwa wakati wananmchagua hawakugalia sifa za mtu wanayemchagua na kuwianisha na changamoto zao ili kujua kama anaweza kuwa ni aina ya kiongozi wanayemhitaji.
Kwamba huenda walimchagua kwa kuwa ni mtu maarufu jimboni kwao, au ni tajiri sana, au ni ndugu yao, au aliwahonga sana kuliko wagombea wenzake, au alikuwa anapigiwa kampeni na watu wanaowaheshimu sana humo jimboni, nikamweleza hizo zote na zingine za kufafana nazo siyo sifa na wala hazitakaa ziwe sifa za kiongozi bora.
Na hicho ndicho huwa tunakifanya Watanzania tunapoingia katika vyumba vya kupigia kura, iwe katika uchaguzi wa kura za maoni au uchaguzi mkuu, tunatumia vigezo vya ajabu sana na kwa kweli, ashakum si matusi, ni vya kipumbavu kuchagua viongozi wetu.
Mwaka huu kama kweli ile kiu ya mabadiliko iliyopo ni ya kweli, kama sio unafiki, basi ni lazima Watanzania katika ngazi zote bila kujali kiwango cha elimu ya mtu, aina ya kazi unayofanya au mahali unapoishi, tubadilike kwanza sisi wenyewe na tuwe tayari kulipa gharama za mabadiliko.
Hivi kuna haja gani ya kuwa na mbunge kwa miaka 10 au zaidi lakini ambaye hana mchango wowote wa maana kwa maendeleo ya jimbo, naomba nieleweke ninaposema maendeleo ya jimbo, sizungumzii vijizawadi na vitakrima vinavyotolewa kwa viongozi wenu wa matawi au kata, au hata kwa baadhi ya watu maarufu, ambavyo mimi ninaviita ni vijirushwa katika ngozi ya zawadi.
Maendeleo ninayozungumzia hapa ni ya jumla na yanayofaidisha jamii nzima kama maji, barabara, elimu na huduma zingine za jamii ambazo kila mwanajimbo anaweza kujivunia kuwa hakupoteza kura yake bure.
Na kuleta mchango katika hili siyo lazima mtu awe na pesa za kutoa mfukoni, kwanza mtu mwenye kutoa pesa mfukoni kwa ajili ya maendeleo ya jimbo, huyo hafai na hana sifa za kuwa kiongozi, mchango ninaouzungumzia mimi hapa ni jinsi anavyowaunganisha wanajimbo kuweza kuzikabili changamoto zenu kwa kutumia rasilimali chache mlizonazo ili kuweza kujikwamua na hali mliyomo na kupiga hatua.
Chonde chonde Watanzania, mwaka huu ni wa ukombozi, tusipige kura kwa mazoea, tuchague aina ya mtu ambaye tunaamini anaweza kuwa msaada kwetu na siyo kwa kuwa eti ni tajiri sana, tukubali kuwa chanzo cha mabadiliko tunayoyatamani. Unapopiga yowe la Kamata mwizi! Kamata mwizi! ni sharti na wewe uwe nyuma ukimfukuza mwizi huyu kwa juhudi kubwa, ndipo wengine watakuunga Mkono.
Kadhalika mabadiliko na ukombozi wa kweli wa nchi hii unahitaji mapinduzi ya kweli, siyo ya mtutu wa bunduki wala mapanga, bali kwa sanduku la kura, ambayo lakini yatatokana na kubadilika kwa mtazamo wetu wakati wa kupiga kura.
Mungu ibariki Tanzania
drbugaywa@yahoo.com, 0754 449 421

Friday, February 5, 2010

CCM, mchelea mwana kulia…!

Na Deus Bugaywa



Chama Cha Mapinduzi leo kinatimiza miaka 33 tangu kuzaliwa kwake tarehe 5, Februari, 1977 baada ya kuungana kwa vya vya TANU na ASP na kuunda chama kimoja kilichoitwa cha Mapinduzi.

Kiliunda cham kipya kikiwa ni mrithi wa wazazi wake waliokitangulia ambao kwa namna moja ama nyingine walihusika na ukombozi wa Tanzania na kutuwezesha kupata uhuru toka wa Mkoloni na Usultani wa kiarabu kwa Zanzibar.

Hiki ni chama ambacho kiliundwa kwa makusudi maalum ya kuwatetea wakulima na wafanyakazi wa Tanzania , kilikuwa na malengo mahsusi ya kumkomboa mwananchi mnyinge kutoka katika unyonge wake na kumfanya mtu anayetahamniwa.

Kwa sababu madhumuni ya kupigania uhuru hayakuwa kumwondoa tu mkoloni wa kizungu ndio unyonge wa mwafrika wa Kitanzania utakuwa umekwisha, ndio maana kikaundwa chama hiki ili kumwezesha mwananchi huyo kupata na kuweza kuiishi tafsiri na maana halisi ya kuwa uhuru.

Kwa maana nyingine CCM kiliundwa ili kiweze kumwzesha Mtanzania kujikinga na wimbi la wanyonyaji na walanguzi wa wakati huo ambao waliona na kamiani kwamba mafanikio yao hayawezi kuja bila kuwafanya watu wengine kuwa dhalili.

Kwa hiyo siyo bahati mbaya kwamba moja ya misingi iliyokiundiwa chama hiki iliyolithiwa toka TANU ni msingi wake wa kwanza unaowataka wanachama wake kuamini kwa dhati kwamba binadmau wote ni sawa na ndugu zangu na Afrika ni moja.

Tena ikasisitizwa kwamba pale mtu anapopewa heshima ya kuwangoza au kuwatumikia Watanzania wenzake asijione kuwa ndiyo amekuwa ‘mkoloni mweusi’ wa kuwanyasa wenzake au kutumia mali ya umma kama vile ni mali yake binafsi.

Hawa wakakukbushwa kuwa cheo ni dhamana na wakatakiwa kutotumia vyeo hivyo kwa manufaa yao binfasi isipokuwa kwa ajili ya utumishi na maslahi ya umma na ni umma tu ndio unaotakiwa ufaidike na utumishi wa mtumishi huyu wa umma na vinginevyo.

Bila shaka tutkubaliana kwamba msingi mwingine muhimu katika ukuaji na hatimaye kufikiwa malengo ya taasisi au chama chochote kile ni ukweli, kwa maana na tasira zake zote, wana CCM hapa walisisitizwa kusema kweli daima na fitina kwao iwe mwiko.

Hii na Minsingi mingine imekifanya chama hiki leo kufikia umri huu na kukifanya moja vyama vikongwe kabisa vya siasa sio tu katika Tanzania lakini pia ndani ya bara la Afrika.

Bila shaka wana CCM wanahitaji pongezi hili, kufikia umri huu ni kazi kubwa mabyo siyo vyama vingi vyenye lika moja an CCM vimeweza kufikisha umri huo vikiwa bado ni vyama tawala. Kwa hili tu wanastahili pongezi hata kama namna ya kufikisha kwao umri huu kunahitaji mjadala lakini walau wafika.

Pamoja na pongezi hizo, hata hivyo, ni jambo jema pia kwa wenye chama chao hiki, kuongozwa na hekima ya kawaida kabisa katika maisha haya kwamba, kitu cha muhimu katika maisha haya siku zote siyo pale ulipo isipokuwa ni wapi nuanelekea.

Mtu yeyote makini habweteki na kufika pale alipofika, isipokuwa anakaza mwendo kuweza kuongeza nguvu na kurekebishwa mwelekeo wake ili asiende kombo. Atatumia uzoefu, kwa kutahimini uwezo na mapungufu aliyokuwa nayo katika kufika hapo alipofika.

Ndio maana ni muhimu kwa wanachama wa chama hiki wanapofurahia siku ya kuazaliwa kwa chama chao, wajiulize swali wana umbali gani wa kwenda wakiwa katika furaha hii ya sasa?

Watakubaliana na mi kwamba wamefika hapa kutokana na misingi imara iliyosimamiwa na uongozi thabiti wa chama hicho, ambao sina hakika sana kama wanaweza wakasimama kifua mbele wakasema wanao uongozi wa aina hiyo ndani ya chama chao kwa sasa unaweza hata kushabihiana kwa nusu wa ule uliowaasisi na kuwawezesha kuweza kusafiri safari hii ndefu mpaka hapa walipo leo.

Wenyewe ni mashahidi wa jinsi ambavyo mpaka hapa walipofika bado wanasafiria kivuli cha utahbiti wa viongozi waasisi wao hata baada ya miongo miwili kupita tangu kiazi chao kipya kiakbiziwe chama.

Alichofanikiwa kwa kiasi kikubwa ni kuivunja vunja miiko hiyo n badala yake sasa chama kimekosa ile maana yake halisi ya kuwa kundi la watu wenye dhamira na nia moja katika kutekeleza malengo yanayofanana.

Leo katika CCM wapo wanachama mahiri wengi tu lakini, kama si mnafiki huwezi kukiita chama hicho ni kimoja kwa hali ilivyo sasa. Ni kundi moja ambalo lakini kila mwana kikundi anasababu zake tofauti kabisa na mwenzake za kuwemo ndai ya kundi hilo na namna tofauti kabisa tena zinazokinzana za kueteleza malengo hayo.

Ni kama timu inayoundwa na wachezaji wazurina mahili wa kimataifa lakini ambao hawana ushirikiano wa kitimu ‘team work’. Kila mchezaji anakuwepo pale isyo kwa ajili ya kufunga magoli lakini kwa ajili ya kuonyesha jinsi alivyo mtaalam kulamba chenga maadui zake, na kuwaonyesha maadui zake (wa ndani na nje ya timu) namna anavyoweza kumudu mpira, lakini ujuzi huo haumsaidii kufunga magoli.

Ndiyo umvyoweza kuiliezea CCM ya sasa, ambayo pamoja na kusherekea umri huo uliotukuka ukilinganisha na vyama vingine vya siasa nchini, kwa hakika badao kinaoneka kana kilizaliwa baada ya mfumo wa vyama vingi, na kwamba labda ndio kinajifunza siasa. Ukikitazama kwa makini kwa kweli huwezi ukaona umri wake unaakisiwa katika namna kinavyojiedesha.

Kwanini kimefika hapa, bila shaka ni kutokana na kutosikia la mkuu na hivyo kinajikuta taratibu na kwa uhakika kinapoteza miguu. Wahenga wetu wamewahi kutuonya kuwa ‘Mchelea Mwana kulia, hulia yeye’.

Kwamba ukiwa wewe ni mlezi wa mtoto halafu anapofanya kosa hutaki kumkanya kwa vile unaogopa atalia basi wewe ndiyo ujiandae kulia. Na hiki ndicho kilichoikuta CCM.

Kumekuwa na ungonjwa mbaya kabisa usiofaa wa kulindana ndani ya chama hiki, mtu akifanya kosa ambalo kwa tartaibu za kawaida tu ama anatakiwa awajibike au kama si muungwana anakuwa na kiburi hataki kuwajibika basi awajibishwe na mamlaka anayowajibika kwayo.

Hili limekuwa haliwezekani ndani ya chama, kiemfika mahali kinadhani kwamba ni chenyewe tu chenye hati miliki ya kutawala nchi hii, na zaizi sana kinadhani Watanzania wote ni wajinga kiasi kwamba wanaweza kuafanya madudu yao halafu wakaendelea kuaminika tu na wananchi kwa kiwango kile kile, hili ni kosa moja kubwa wanalofanya CCM.

Kiongozi wa chama anapokosea au anapopatikana na kashfa ambazo zinaweza kuharibu sifa na jina la chama kwa wananchi utasikia viongozi wa cham tena wengine wa kitaifa eti wakikitetea chama kwamba huyu aliyefanya hivyo mwanachama wa CCM siyo CCM.

Halafu mtu huyu hata hawajiishwi walau kisiasa ili kweli chama kiwezi kujitenga nae na wananchi wajue kweli kwamba kimejitenga na mkosaji au mtuhumiwa huyo, lakini kuendelea kumkana mtuhumiwa halafu upande wa pili kinaendelea kumkumbatia, huko ni kujiandalia mauti.

Ni vyema, kama inataka kuendelea kuishi, CCM ikajifunza kwa wazee wenzake Kenya , Zambia , Malawi ili irekebishe makosa yake. Kila lakheri CCM katika umri huu

drbugaywa@yahoo.com 0754 449 421

Uharamia Ziwa Victoria na hatma yetu

Na Deus Bugaywa



Historia au uzoefu, ilisemwa, ni mwalimu mzuri sana hasa kwa wanafunzi makini na wanaothamini maana ya kujifunza. Kwa kuwa kila kinachotokea katika maisha yao kiwe kibaya au kizuri kinakuwa ni somo murua ambalo linawafanya ama waweke mbinu za kukiendeleza chema hicho au mikakati ya kuakabiliana na kukomesha chochote kibaya kilichotokea.

Inawezekana sisi, Tanzania , bahati hii ya kuwa wanafunzi makini wa uzoefu na historia imetupita kushoto na kwa hiyo tunaishi tu ili mradi kunakucha na maisha yanaendelea ama kwa wema au ubaya, potelea mabali Mungu ndiye ajuaye.

Pengine sisi ni mfano halisi wa jamii zile zinazoongozwa na msemo ya wahenga wetu kwamba kwenye miti hapa wajenzi, kuna wafunga fito tu. Nazungumzia juu ya usimamizi wa rasilimali zetu na jinsi mabayo zinaweza kutuletea anufaa yanayoshabihiana kweli na umiliki wetu wa rasilimali hizo.

Jinsi mabavyo rasilimali hizi zinaweza kunufaisha mwananchi Mtanzania mwenye bidii ya kazi ambaye ameamua kutumia rasilimali ambazo taifa hililimejaliwa kuwa nazo kuyafanya maisha yake yawe ya kiutu, heshima na hadhi ya binadamu anayeheshimika na kuthaminiwa.

Moja ya tunu ambazo Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema, ametujalia ni pamoja na kuwa wamiliki wa sehemu zaidi ya nusu ya Ziwa kubwa kuliko yote katika Afrika na la pili kwa Ukubwa duniani baada ya Ziwa Superior liliko Kaskazini mwa Amerika, ninazungumzia Ziwa Victoria .

Ziwa hili lenye ukubwa wa kilomota za mraba zipatazo 68, 800 limetuunganisha na nchi mbili za Afrika Mashariki za Kenya na Uganda kwa uwiano wa umiliki wa Tanzania asilimia 51, Uganda asilimia 43 na Kenya asilimia 6.

Licha ya kuwa Ziwa hili ni chanzo muhimu cha maji kwa wakazi wanaoishi ndani ya bonde la Ziwa Victoria, pia ni chanzo muhimu cha malighafi za viwada vya samaki na mazao yake, kilimo cha umwagiliaji, uvuvi na shughuli nyingine nyingi, zinazolifanya Ziwa hili kuwa tumaini la maisha kwa watu wapatao milioni 30 wanaoishi katika bonde lake, bado hali ya usalama wa watu na mali zao siyo nzuri.

Hali ya usalama ndani ya Ziwa hili linabaki kuwa changamoto kubwa kwa serikali, jeshi la polisi na wananchi kwa ujumla kwa kuwa hakuna anayeweza kusema hahusiki moja kwa moja na hali ya kukosekana kwa usalama ndani ya Ziwa hili.

Mazingira na miundombinu ya visiwa vingi vilivyoko ndani ya ziwa, vikiwemo vyenye makazi ya kudumu na vingine vinavyokaliwa na wavuvi kwa misimu kama kambi za uvuvi ni moja ya changamoto kubwa katika kuhakikisha usalama ndani ya ziwa hili.

Utete wa usalama unachangiwa pia na kuwa na mipaka inayotenganisha nchi zetu tatu ndani ya Ziwa ambako wakati mwingine, bila ushirikiano wa dhati kutoka kwa nchi zote zinazougana ndani ya ziwa katika kuimarisha ulinzi, udhibiti wa uharamia linakuwa ni suala gumu sana .

Si hivyo tu upana wake pia na dhana duni za askari wetu hasa katika kukabiliana na uhalifu kwenye mazingira kama hayo ya majini nayo ni moja ya chanagmoto kubwa sana .

Urefu wa Ziwa hili toka Kaskazini hadi Kusini ni kilomita 337 na upana wake toka Mashariki mpaka Magharibi ni kilomita 240, katika hali ya upana wa namna hii na kuwepo kwa visiwa vingi na ambavyo ni vituo muhimu kwa shughuli za uvuvi na uduni wa vyombo vya doria ndani ya ziwa vinalifanya kuwa sehemu salama sana kwa wezi na maharamia.

Itakubukwa kwamba upo wakati, kuna baadhi ya watu wenye pesa ambao walijitangazia ‘vijamhuri’ vyao kwenye baadhi ya visiwa, wao ndio wakawa ‘serikali’ za visiwa hivyo. Serikali mkoa wa Mwanza ilikanusha sana habari hizi, ingawa hili halikuondoa ukweli.

Watu hawa, wenye pesa na mtandao mpana, walikuwa wanaendesha visiwa hivyo na kuwafanya wavuvi kama mali yao , kwa kuwa ndani ya visiwa hivyo kwa mujibu wao ‘hakuna serikali’.

Vitendo vya kikatili na kinyama ndani ya ziwa hili kweli vingeweza kukusadikisha kweli kwamba serikali haipo huko. Kuvamiwa kwa wavuvi na kuzamishwa majini huku majambazi hao wakijichukulia kila kitu, ulikuwa ni utaratibu wa kawaida, Kulikuwa na mtandao mkubwa ambao ulikuwa na kazi ya kuiba mitumbwi ya injini ambao ulikuwa na matawi yake mpaka Kigoma, hapa jeshi la polisi lilifaniwa walau kuuyumbisha mtandao huu kwa kuwakamata baadhi ya wahusika hali ikawa shwari kidogo, sina hakika kaa umekufa.

Uko mtindo uliokuwa maarufu sana ziwani humu, ambao unaitwa ‘Car wash’ au ‘kaptula’, hii ilikuwa inamaanisha maharamia wanapowavamia wavuvi wanawataka ama wachague kukatwa mikono na mabega (car wash) au miguu (kaptula). Hapa napo wavuvi waliteseka vya kutosha.

Ninachokikusudia hapa ni kueleza ukweli kwamba hali ya usalama katika ziwa hili ni tete sana na halijawahi kuwa salama isipokuwa ukatili na unyama huu unabadili sura tu.

Tukio la hivi majuzi katika Kisiwa cha Izinga lilipoteza maisha ya Watanzania 13 na kujeruhi wengine 17 ni ya aina nyingine tu ya jinsi ukatili katika ziwa hili unaweza kuvaa sura mbali mbali.

Kinachotakiwa ni kuweka mikakati ambayo itasaidia kuhakikisha usalama wa watu na mali zao ndani ziwa hili na kulifanya kuwa ukanda muhimu wa uzalishaji mali kwa ustawi wa watu wetu na taifa letu kwa ujumla na siyo kualichia taratibu kugeuka kuwa kaburini na chanzo cha umaskini, ulemavu na mauti kwa Watanzania.

Ni kweli kwamba Operesheni maalum kama hii inayoendeshwa sasa ndani ya Ziwa hilo na Kamanda Tossi iliyopewa jina la ‘Operesheni Chakaza’ ni muhimu kwa ajili ya kutuliza hali ya mambo na kuwakamata watuhumiwa wa mauaji ili wafikishwe mbele ya mkono wa sheria.

Pamoja na umhimu huo, operesheni hizi haziwezi kwa zenyewe tu kurejesha hali ya utulivu na usalama ambao watu wanauhitaji kwa ajili ya kujiletea maendeleo kwa shughuli za uvuvi na zingine zinazofanyika ziwani humo na kwenye visiwa vyake.

Wananchi pia wanatakiwa kuwa ndio walinzi namba moja wa maslahi yao , kwa kutoa ushrikiano kwa vyombo vya ulinzi, kwa kutoa taarifa kwa watu wanaowahisi wana nyendo zinazoashiria mashaka.

Kwa kuwa ni lazima pia tukiri kwamba kama jinsi miundo mbinu ya ziwa na visiwa hivyo ilivyo na ugumu katika kuimarisha ulinzi wa Ziwa hilo ndivyo pia ilivyo vigumu kwa maharamia kukamilisha mipango yao ya uhalifu, wanafanikiwa kwa kuwa wanapewa ushirikiano na rai wenyeji wasio wema.

Tukiacha kushirikiana nao, na tukiamua kuwadhibiti hawa wachache wanaoshirikiana na majambazi hawa, tunaweza kabisa kudhibiti hali ya usalama wetu bila gharama kuwa na ugumu usiokuwa wa lazima.

Bila kuchukua hatua hizi, tutaendelea kuzifanya rasilimali zetu kama iliyo kwenye madini, kuwa vyanzo vya laana na mauti badala ya kuwa neema kwa hatma ya Tanzania ya leo na ijayo.

Mungu ibariki Tanzania

0754 449 421 drbugaywa@yahoo.com

Ukombozi Tanzania uko mikononi mwako

Na Deus Bugaywa



Ni kweli kwamba maendeleo katika sehemu yeyote duniani yanaletwa na watu wenyewe, kwamba hakuna muujiza unaoweza kujitokeza kumletea mtu maendeleo isipokuwa kwa kufanyakazi kwa bidii na maarifa.

Lakini katika Afrika na Tanzania ukiwa mmoja wa mifano halisi imedhirika sasa kwamba viongozi wana mchango mkubwa sana katika kuwa chanzo cha matatizo na umaskini mkubwa kwa watu wake.

Umaskini na matatizo ya taifa na wananchi unatokomezwa kwa mipango na mikakati mahsusi inayopangwa na kutekelezwa kwa makini na viongozi shupavu na wenye uzalendo wa kweli kwa taifa lao.

Viongozi wa aina hii ni wale tunaowaita viongozi watumishi, ni aina ya viongozi ambao wanajua wao ni watumishi tu wa umma wa jamii wanayoingoza, na hivyo wanaheshimu na kuthamini dhamana walizopewa na watu wao.

Katika nchi zetu hizi uongozi ni suala tete sana , ni mchanganyiko wa watu wa aina mbali mbali ambao wengine hata hawana hata chembe ya sifa ya kuitwa viongozi. Ni ndoto ya kila mwananchi kuwa na viongozi bora ambao hawa wanaweza kuleta matumaini kwa watu wao, ya kulirejesha taifa katika njia ambayo inaweza kusaidia kulikwamua taifa kuondokana na umaskini uliopindukia.

Kwa upande mwingine wapo viongozi wabovu ambao kwa uongozi ni njia ya makato kufikia enzi na heshima ya utukufu wa utajiri kwa njia ambazo siyo halali. Kwao kutumia kila aina ya hila na mbinu chafu kujinufaisha kwa gharama za umaskini wa wananchi waliowapa dhamana hizo.

Wananchi wengi kwa sasa wanajua wazi na kwa uhakika jinsi ambavyo viongozi wanapuuza sauti zao dhidi ya rushwa, wanajua jinsi vingozi waivyowageuza ngazi za kupandia kuuendea ufalme wa ukwasi mkubwa katikati ya lindi kubwa la umaskini.

Kama tunakubalina kimsingi kwamba kuendela au kutoendelea kwa taifa kunategemea kwa kiasi kikubwa sera na mipango taifa iliyojiwekea na upeo wa viongozi wake waliopewa jukumu la usimamizi wa rasilimali za taifa.

Tukiwa tunaelekea katika uchaguzi mkuu baadae Mwezi oktoba mwaka huu, ni lazima kama wananchi wa taifa hili tukae na kufanya tafakuri makini juu ya hatma ya taifa letu.

Uko ukweli wa hakika kwamba fikra, tabia na mienendo na mazoea yaliyotuingiza katika matatizo tuliyo nayo kwa sasa kama taifa, hasa ya usimamizi mbaya kabisa wa rasilimali zetu hayawezi kutusaudia kuyatatua matatizo haya, kwa kifupi ni kwamba mfumo uliotuingiza katika matatizo haya hauwezi kututoa katika matatizo hayo.

Tunahitaji mfumo mpya na fikra za kimapinduzi ili kuweza kutumia vyema fursa ya kuweka viongozi katika madaraka, ni lazima historia itufundishe na kama tusipokubali kuwa wanafunzi wazuri wa historia yetu wenyewe, hatutakuwa na budi ila kuvunjika guu.

Watanzania tumekuwa na tabia ya kufanya chaguzi zetu kwa mazoea tu bila kuwa na agenda mahsusi na kujiuliza swali ya msingi ya kwanini tunafanya uchaguzi. Tunauona kila uchaguzi kama ni tukio la kawaida tu ambalo linakuja na kupita kama yanavyokuja matukio mengine yote.

Lakini ni vyema mwaka huu tukaamua kubadilika, kw amantiki kwamba mpaka tutakapobadilika sisi wenyewe waannchi mmoja mmoja, hatuwezi kutarajia mabadiliko kutoka kwa viongozi wetu.

Ni kweli kwamba baadhi ya viongozi hawa wamekuwa ndio chanzo cha matatizo yetu, kwa kukosa kwao umakini, kutingia katika mikataba isiyo na maslahi kwa taifa, kuendekeza rushwa na ufisadi, na kutothamini dhamana zao na wakati mwignine uwezo mdogo wa kuongoza.

Abraham Lincoln alipoitafsiri Demokrasia kuwa Serikali ya watu, inayotokana na watu kwa ajili watu hao hao, hakuwa na maana nyignine isipokuwa watu wachague viongozi ambao watukuwa wanaendesha serikali wa matakwa na amslahi ya watu wenye taifa husika waliowachagua viongozi hao.

Kwa hiyo uchaguzi kwa maana nyingine ndio njia pekee anaypata fursa mwananchi kuamua serikali yake iendeshweje na nani aiendeshe serikali hiyo. Hapa kura inakuwa na ngvu na mamlaka makubwa kuliko bunduki au kombora lolote lile.

Bahati yetu mbaya ni kwamba wananchi wengi hatujajuwa au sijui ni kwa kusudi tu, tunaamua kutumia kura zetu kama karata za kuchezea kamari, halafu baada ya uchaguzi au kiongozi akishakuwa tayrai kwenye hatamu za uongozi tunamuogopa anatuburuza anavyotaka na kujichotea rasilimali zetu kama zisizokuwa na mwenyewe halafu tunabaki tunalalamika na kunung’unika kana kwamba hapo alipo kajiweka.

Huu ni wakati wa Watanzania kujitambua na kuujua udhaifu wetu ulipo na kujua nguvu yetu iko wapi, ni lazima tuujue na kuukubali ukweli kwamba malalamiko na manug’uniko hajawahi kutatua tatizo lolote hapa duniani, kwa hiyo tunaweza kusema kulalamika na kunun’gunika kuwa wanyonge wa nchi hii bila kuchukua hatua ni unafiki na dhambi isiyostahili msamaha.

Ni muhimu kutambua kuwa uchaguzi au kura yetu ina maana kubwa sana, hiyo ndiyo elimu ya watoto wetu, kama una kero na kesi nyingi za ardhi mabazo hazina ufumbuzi, halamshauri yako unaishuhudia jinsi inavyonuka rushwa na jinsi wnaanchi mnavyookena kero na takataka unapokwenda kushughulikia suala lako la ardhi, iwe kupimiwa au kununua kiwanja, hapo utambue kuwa, hapo ujue hauna diwani.

Wala huhitaji kumlalamikia mtu tambua kwamba jicho lako ulilolipelekea kukumulikia ndani ya halamshauri yako na kusimamia watendaji wanaokunyanyasa kama mkimbizi ndani ya nchi yako, ama ni bovu au limepofuka kabisa, na jicho hilo haliwezi kuwa jingine isipokuwa diwani wako.

Huyo atakuwa ama hana uwezo wa kupambana na kuwasimamia vyema watendaji wabovu na wala rushwa au kaamua kujinga nao kwa kuwa ufisadi nchi hii kwa sasa ‘unalipa’ na wewe mwananchi unayefisadiwa unaona ndiyo ujanja, unaubariki na kuushabikia.

Hali inapanda ngazi hivyo hivyo kutoka kwenye halmsahauri mapka kwenye taifa, ukiona elimu ya nchi inazidi kuporomoka, waziri anajiendeshea wizara kama ka NGO kake, mitihani inaibwa barazani kama watoto wa darsa la pili wanavyoibiana kalamu za risasi na vifutio, halafu watendaji wakuu wanaendelea kutamalaki ndani ya mamlaka ya baraza la mitihani, hapo ujue kurunzi (mbunge) yako uliyoipeleka kwenye lile jumba la kifalme pale makao makuu ya kusadikika ya nchi, kuimurika serikali ikutumikie vyema ama imezima ahaina betri au imeribika ahitengenezeki, unatakiwa kuchukua hatua za haraka kufanya mabadiliko.

Wanafalsafa wanasema ‘Politics are too serious matters to be left to politicians alone’ kwamba siasa ni jambo nyeti na muhimu sana kuachwa wanasiasa peke yao . Kwa hiyo harakati za siasa zinazoendelea sasa kaika kila kona ya nchi, hata kama huhusishwi zinakuhusu sana , anza kuzifuatilia na ufikie uamuzi muafaka kujibu maswali yako ambayo huna hata wa kumuuliza.

Wakati mwingine utandawazi utusaidie kjifunza baadhi ya mambo mazuri, isiwe kuiga uvaaji wa nguo za ajbau na tabia zinazokinzana na uafrika wetu tu, tunaweza pia kuutumia vizuri.

Wananchi wa Massachusetts juzi wamemwonyesha Rais Obama gharama za kutotimiza ahadi zake kwa kipindi cha mwaka mmoja tu, sisi tunashundwa vipi kuwapa somo hilo hilo madiwani amabo wamekuwa wakituahidi kwa miak nenda rudi, tunashidnwa nini kuwaadabisha wabunge ambao wamegeuka kama nembo za majimbo yetu lakini hawana jipya, tunahindwa nini kutumia kipimo hicho hicho kumpima rais wetu kama kwa miaka hii mitano anayomalizia anatufaa kuendelea au la?

Uchaguzi ni kuchagua mustakabali wetu kama taifa, kila tunapompima mtu tumpime kwa vigezo vya hatma na majaliwa ya Tanzania , kutumia vigezo vya urafiki, mwenzetu au mazoea tu, ni kulinyesha sumu ya mamba taifa letu. Inawezekana tutimize wajibu wetu.

Mungu ibariki Tanzania , wabariki na watu wake wajitambue.

drbugaywa@yahoo.com 0754 449 421