Friday, February 5, 2010

Ukombozi Tanzania uko mikononi mwako

Na Deus Bugaywa



Ni kweli kwamba maendeleo katika sehemu yeyote duniani yanaletwa na watu wenyewe, kwamba hakuna muujiza unaoweza kujitokeza kumletea mtu maendeleo isipokuwa kwa kufanyakazi kwa bidii na maarifa.

Lakini katika Afrika na Tanzania ukiwa mmoja wa mifano halisi imedhirika sasa kwamba viongozi wana mchango mkubwa sana katika kuwa chanzo cha matatizo na umaskini mkubwa kwa watu wake.

Umaskini na matatizo ya taifa na wananchi unatokomezwa kwa mipango na mikakati mahsusi inayopangwa na kutekelezwa kwa makini na viongozi shupavu na wenye uzalendo wa kweli kwa taifa lao.

Viongozi wa aina hii ni wale tunaowaita viongozi watumishi, ni aina ya viongozi ambao wanajua wao ni watumishi tu wa umma wa jamii wanayoingoza, na hivyo wanaheshimu na kuthamini dhamana walizopewa na watu wao.

Katika nchi zetu hizi uongozi ni suala tete sana , ni mchanganyiko wa watu wa aina mbali mbali ambao wengine hata hawana hata chembe ya sifa ya kuitwa viongozi. Ni ndoto ya kila mwananchi kuwa na viongozi bora ambao hawa wanaweza kuleta matumaini kwa watu wao, ya kulirejesha taifa katika njia ambayo inaweza kusaidia kulikwamua taifa kuondokana na umaskini uliopindukia.

Kwa upande mwingine wapo viongozi wabovu ambao kwa uongozi ni njia ya makato kufikia enzi na heshima ya utukufu wa utajiri kwa njia ambazo siyo halali. Kwao kutumia kila aina ya hila na mbinu chafu kujinufaisha kwa gharama za umaskini wa wananchi waliowapa dhamana hizo.

Wananchi wengi kwa sasa wanajua wazi na kwa uhakika jinsi ambavyo viongozi wanapuuza sauti zao dhidi ya rushwa, wanajua jinsi vingozi waivyowageuza ngazi za kupandia kuuendea ufalme wa ukwasi mkubwa katikati ya lindi kubwa la umaskini.

Kama tunakubalina kimsingi kwamba kuendela au kutoendelea kwa taifa kunategemea kwa kiasi kikubwa sera na mipango taifa iliyojiwekea na upeo wa viongozi wake waliopewa jukumu la usimamizi wa rasilimali za taifa.

Tukiwa tunaelekea katika uchaguzi mkuu baadae Mwezi oktoba mwaka huu, ni lazima kama wananchi wa taifa hili tukae na kufanya tafakuri makini juu ya hatma ya taifa letu.

Uko ukweli wa hakika kwamba fikra, tabia na mienendo na mazoea yaliyotuingiza katika matatizo tuliyo nayo kwa sasa kama taifa, hasa ya usimamizi mbaya kabisa wa rasilimali zetu hayawezi kutusaudia kuyatatua matatizo haya, kwa kifupi ni kwamba mfumo uliotuingiza katika matatizo haya hauwezi kututoa katika matatizo hayo.

Tunahitaji mfumo mpya na fikra za kimapinduzi ili kuweza kutumia vyema fursa ya kuweka viongozi katika madaraka, ni lazima historia itufundishe na kama tusipokubali kuwa wanafunzi wazuri wa historia yetu wenyewe, hatutakuwa na budi ila kuvunjika guu.

Watanzania tumekuwa na tabia ya kufanya chaguzi zetu kwa mazoea tu bila kuwa na agenda mahsusi na kujiuliza swali ya msingi ya kwanini tunafanya uchaguzi. Tunauona kila uchaguzi kama ni tukio la kawaida tu ambalo linakuja na kupita kama yanavyokuja matukio mengine yote.

Lakini ni vyema mwaka huu tukaamua kubadilika, kw amantiki kwamba mpaka tutakapobadilika sisi wenyewe waannchi mmoja mmoja, hatuwezi kutarajia mabadiliko kutoka kwa viongozi wetu.

Ni kweli kwamba baadhi ya viongozi hawa wamekuwa ndio chanzo cha matatizo yetu, kwa kukosa kwao umakini, kutingia katika mikataba isiyo na maslahi kwa taifa, kuendekeza rushwa na ufisadi, na kutothamini dhamana zao na wakati mwignine uwezo mdogo wa kuongoza.

Abraham Lincoln alipoitafsiri Demokrasia kuwa Serikali ya watu, inayotokana na watu kwa ajili watu hao hao, hakuwa na maana nyignine isipokuwa watu wachague viongozi ambao watukuwa wanaendesha serikali wa matakwa na amslahi ya watu wenye taifa husika waliowachagua viongozi hao.

Kwa hiyo uchaguzi kwa maana nyingine ndio njia pekee anaypata fursa mwananchi kuamua serikali yake iendeshweje na nani aiendeshe serikali hiyo. Hapa kura inakuwa na ngvu na mamlaka makubwa kuliko bunduki au kombora lolote lile.

Bahati yetu mbaya ni kwamba wananchi wengi hatujajuwa au sijui ni kwa kusudi tu, tunaamua kutumia kura zetu kama karata za kuchezea kamari, halafu baada ya uchaguzi au kiongozi akishakuwa tayrai kwenye hatamu za uongozi tunamuogopa anatuburuza anavyotaka na kujichotea rasilimali zetu kama zisizokuwa na mwenyewe halafu tunabaki tunalalamika na kunung’unika kana kwamba hapo alipo kajiweka.

Huu ni wakati wa Watanzania kujitambua na kuujua udhaifu wetu ulipo na kujua nguvu yetu iko wapi, ni lazima tuujue na kuukubali ukweli kwamba malalamiko na manug’uniko hajawahi kutatua tatizo lolote hapa duniani, kwa hiyo tunaweza kusema kulalamika na kunun’gunika kuwa wanyonge wa nchi hii bila kuchukua hatua ni unafiki na dhambi isiyostahili msamaha.

Ni muhimu kutambua kuwa uchaguzi au kura yetu ina maana kubwa sana, hiyo ndiyo elimu ya watoto wetu, kama una kero na kesi nyingi za ardhi mabazo hazina ufumbuzi, halamshauri yako unaishuhudia jinsi inavyonuka rushwa na jinsi wnaanchi mnavyookena kero na takataka unapokwenda kushughulikia suala lako la ardhi, iwe kupimiwa au kununua kiwanja, hapo utambue kuwa, hapo ujue hauna diwani.

Wala huhitaji kumlalamikia mtu tambua kwamba jicho lako ulilolipelekea kukumulikia ndani ya halamshauri yako na kusimamia watendaji wanaokunyanyasa kama mkimbizi ndani ya nchi yako, ama ni bovu au limepofuka kabisa, na jicho hilo haliwezi kuwa jingine isipokuwa diwani wako.

Huyo atakuwa ama hana uwezo wa kupambana na kuwasimamia vyema watendaji wabovu na wala rushwa au kaamua kujinga nao kwa kuwa ufisadi nchi hii kwa sasa ‘unalipa’ na wewe mwananchi unayefisadiwa unaona ndiyo ujanja, unaubariki na kuushabikia.

Hali inapanda ngazi hivyo hivyo kutoka kwenye halmsahauri mapka kwenye taifa, ukiona elimu ya nchi inazidi kuporomoka, waziri anajiendeshea wizara kama ka NGO kake, mitihani inaibwa barazani kama watoto wa darsa la pili wanavyoibiana kalamu za risasi na vifutio, halafu watendaji wakuu wanaendelea kutamalaki ndani ya mamlaka ya baraza la mitihani, hapo ujue kurunzi (mbunge) yako uliyoipeleka kwenye lile jumba la kifalme pale makao makuu ya kusadikika ya nchi, kuimurika serikali ikutumikie vyema ama imezima ahaina betri au imeribika ahitengenezeki, unatakiwa kuchukua hatua za haraka kufanya mabadiliko.

Wanafalsafa wanasema ‘Politics are too serious matters to be left to politicians alone’ kwamba siasa ni jambo nyeti na muhimu sana kuachwa wanasiasa peke yao . Kwa hiyo harakati za siasa zinazoendelea sasa kaika kila kona ya nchi, hata kama huhusishwi zinakuhusu sana , anza kuzifuatilia na ufikie uamuzi muafaka kujibu maswali yako ambayo huna hata wa kumuuliza.

Wakati mwingine utandawazi utusaidie kjifunza baadhi ya mambo mazuri, isiwe kuiga uvaaji wa nguo za ajbau na tabia zinazokinzana na uafrika wetu tu, tunaweza pia kuutumia vizuri.

Wananchi wa Massachusetts juzi wamemwonyesha Rais Obama gharama za kutotimiza ahadi zake kwa kipindi cha mwaka mmoja tu, sisi tunashundwa vipi kuwapa somo hilo hilo madiwani amabo wamekuwa wakituahidi kwa miak nenda rudi, tunashidnwa nini kuwaadabisha wabunge ambao wamegeuka kama nembo za majimbo yetu lakini hawana jipya, tunahindwa nini kutumia kipimo hicho hicho kumpima rais wetu kama kwa miaka hii mitano anayomalizia anatufaa kuendelea au la?

Uchaguzi ni kuchagua mustakabali wetu kama taifa, kila tunapompima mtu tumpime kwa vigezo vya hatma na majaliwa ya Tanzania , kutumia vigezo vya urafiki, mwenzetu au mazoea tu, ni kulinyesha sumu ya mamba taifa letu. Inawezekana tutimize wajibu wetu.

Mungu ibariki Tanzania , wabariki na watu wake wajitambue.

drbugaywa@yahoo.com 0754 449 421

No comments:

Post a Comment