Friday, February 5, 2010

Uharamia Ziwa Victoria na hatma yetu

Na Deus Bugaywa



Historia au uzoefu, ilisemwa, ni mwalimu mzuri sana hasa kwa wanafunzi makini na wanaothamini maana ya kujifunza. Kwa kuwa kila kinachotokea katika maisha yao kiwe kibaya au kizuri kinakuwa ni somo murua ambalo linawafanya ama waweke mbinu za kukiendeleza chema hicho au mikakati ya kuakabiliana na kukomesha chochote kibaya kilichotokea.

Inawezekana sisi, Tanzania , bahati hii ya kuwa wanafunzi makini wa uzoefu na historia imetupita kushoto na kwa hiyo tunaishi tu ili mradi kunakucha na maisha yanaendelea ama kwa wema au ubaya, potelea mabali Mungu ndiye ajuaye.

Pengine sisi ni mfano halisi wa jamii zile zinazoongozwa na msemo ya wahenga wetu kwamba kwenye miti hapa wajenzi, kuna wafunga fito tu. Nazungumzia juu ya usimamizi wa rasilimali zetu na jinsi mabayo zinaweza kutuletea anufaa yanayoshabihiana kweli na umiliki wetu wa rasilimali hizo.

Jinsi mabavyo rasilimali hizi zinaweza kunufaisha mwananchi Mtanzania mwenye bidii ya kazi ambaye ameamua kutumia rasilimali ambazo taifa hililimejaliwa kuwa nazo kuyafanya maisha yake yawe ya kiutu, heshima na hadhi ya binadamu anayeheshimika na kuthaminiwa.

Moja ya tunu ambazo Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema, ametujalia ni pamoja na kuwa wamiliki wa sehemu zaidi ya nusu ya Ziwa kubwa kuliko yote katika Afrika na la pili kwa Ukubwa duniani baada ya Ziwa Superior liliko Kaskazini mwa Amerika, ninazungumzia Ziwa Victoria .

Ziwa hili lenye ukubwa wa kilomota za mraba zipatazo 68, 800 limetuunganisha na nchi mbili za Afrika Mashariki za Kenya na Uganda kwa uwiano wa umiliki wa Tanzania asilimia 51, Uganda asilimia 43 na Kenya asilimia 6.

Licha ya kuwa Ziwa hili ni chanzo muhimu cha maji kwa wakazi wanaoishi ndani ya bonde la Ziwa Victoria, pia ni chanzo muhimu cha malighafi za viwada vya samaki na mazao yake, kilimo cha umwagiliaji, uvuvi na shughuli nyingine nyingi, zinazolifanya Ziwa hili kuwa tumaini la maisha kwa watu wapatao milioni 30 wanaoishi katika bonde lake, bado hali ya usalama wa watu na mali zao siyo nzuri.

Hali ya usalama ndani ya Ziwa hili linabaki kuwa changamoto kubwa kwa serikali, jeshi la polisi na wananchi kwa ujumla kwa kuwa hakuna anayeweza kusema hahusiki moja kwa moja na hali ya kukosekana kwa usalama ndani ya Ziwa hili.

Mazingira na miundombinu ya visiwa vingi vilivyoko ndani ya ziwa, vikiwemo vyenye makazi ya kudumu na vingine vinavyokaliwa na wavuvi kwa misimu kama kambi za uvuvi ni moja ya changamoto kubwa katika kuhakikisha usalama ndani ya ziwa hili.

Utete wa usalama unachangiwa pia na kuwa na mipaka inayotenganisha nchi zetu tatu ndani ya Ziwa ambako wakati mwingine, bila ushirikiano wa dhati kutoka kwa nchi zote zinazougana ndani ya ziwa katika kuimarisha ulinzi, udhibiti wa uharamia linakuwa ni suala gumu sana .

Si hivyo tu upana wake pia na dhana duni za askari wetu hasa katika kukabiliana na uhalifu kwenye mazingira kama hayo ya majini nayo ni moja ya chanagmoto kubwa sana .

Urefu wa Ziwa hili toka Kaskazini hadi Kusini ni kilomita 337 na upana wake toka Mashariki mpaka Magharibi ni kilomita 240, katika hali ya upana wa namna hii na kuwepo kwa visiwa vingi na ambavyo ni vituo muhimu kwa shughuli za uvuvi na uduni wa vyombo vya doria ndani ya ziwa vinalifanya kuwa sehemu salama sana kwa wezi na maharamia.

Itakubukwa kwamba upo wakati, kuna baadhi ya watu wenye pesa ambao walijitangazia ‘vijamhuri’ vyao kwenye baadhi ya visiwa, wao ndio wakawa ‘serikali’ za visiwa hivyo. Serikali mkoa wa Mwanza ilikanusha sana habari hizi, ingawa hili halikuondoa ukweli.

Watu hawa, wenye pesa na mtandao mpana, walikuwa wanaendesha visiwa hivyo na kuwafanya wavuvi kama mali yao , kwa kuwa ndani ya visiwa hivyo kwa mujibu wao ‘hakuna serikali’.

Vitendo vya kikatili na kinyama ndani ya ziwa hili kweli vingeweza kukusadikisha kweli kwamba serikali haipo huko. Kuvamiwa kwa wavuvi na kuzamishwa majini huku majambazi hao wakijichukulia kila kitu, ulikuwa ni utaratibu wa kawaida, Kulikuwa na mtandao mkubwa ambao ulikuwa na kazi ya kuiba mitumbwi ya injini ambao ulikuwa na matawi yake mpaka Kigoma, hapa jeshi la polisi lilifaniwa walau kuuyumbisha mtandao huu kwa kuwakamata baadhi ya wahusika hali ikawa shwari kidogo, sina hakika kaa umekufa.

Uko mtindo uliokuwa maarufu sana ziwani humu, ambao unaitwa ‘Car wash’ au ‘kaptula’, hii ilikuwa inamaanisha maharamia wanapowavamia wavuvi wanawataka ama wachague kukatwa mikono na mabega (car wash) au miguu (kaptula). Hapa napo wavuvi waliteseka vya kutosha.

Ninachokikusudia hapa ni kueleza ukweli kwamba hali ya usalama katika ziwa hili ni tete sana na halijawahi kuwa salama isipokuwa ukatili na unyama huu unabadili sura tu.

Tukio la hivi majuzi katika Kisiwa cha Izinga lilipoteza maisha ya Watanzania 13 na kujeruhi wengine 17 ni ya aina nyingine tu ya jinsi ukatili katika ziwa hili unaweza kuvaa sura mbali mbali.

Kinachotakiwa ni kuweka mikakati ambayo itasaidia kuhakikisha usalama wa watu na mali zao ndani ziwa hili na kulifanya kuwa ukanda muhimu wa uzalishaji mali kwa ustawi wa watu wetu na taifa letu kwa ujumla na siyo kualichia taratibu kugeuka kuwa kaburini na chanzo cha umaskini, ulemavu na mauti kwa Watanzania.

Ni kweli kwamba Operesheni maalum kama hii inayoendeshwa sasa ndani ya Ziwa hilo na Kamanda Tossi iliyopewa jina la ‘Operesheni Chakaza’ ni muhimu kwa ajili ya kutuliza hali ya mambo na kuwakamata watuhumiwa wa mauaji ili wafikishwe mbele ya mkono wa sheria.

Pamoja na umhimu huo, operesheni hizi haziwezi kwa zenyewe tu kurejesha hali ya utulivu na usalama ambao watu wanauhitaji kwa ajili ya kujiletea maendeleo kwa shughuli za uvuvi na zingine zinazofanyika ziwani humo na kwenye visiwa vyake.

Wananchi pia wanatakiwa kuwa ndio walinzi namba moja wa maslahi yao , kwa kutoa ushrikiano kwa vyombo vya ulinzi, kwa kutoa taarifa kwa watu wanaowahisi wana nyendo zinazoashiria mashaka.

Kwa kuwa ni lazima pia tukiri kwamba kama jinsi miundo mbinu ya ziwa na visiwa hivyo ilivyo na ugumu katika kuimarisha ulinzi wa Ziwa hilo ndivyo pia ilivyo vigumu kwa maharamia kukamilisha mipango yao ya uhalifu, wanafanikiwa kwa kuwa wanapewa ushirikiano na rai wenyeji wasio wema.

Tukiacha kushirikiana nao, na tukiamua kuwadhibiti hawa wachache wanaoshirikiana na majambazi hawa, tunaweza kabisa kudhibiti hali ya usalama wetu bila gharama kuwa na ugumu usiokuwa wa lazima.

Bila kuchukua hatua hizi, tutaendelea kuzifanya rasilimali zetu kama iliyo kwenye madini, kuwa vyanzo vya laana na mauti badala ya kuwa neema kwa hatma ya Tanzania ya leo na ijayo.

Mungu ibariki Tanzania

0754 449 421 drbugaywa@yahoo.com

No comments:

Post a Comment