Na Deus Bugaywa
Ukiwaangalia Watanzania wa leo utaona kwenye fikra zao, nyuso zao na hisia zao utaona wazi kabisa kuwa iko kiu ya mabdiliko. Watu wanataka mabadiliko wamechoka na mazoea waliokuwa nayo na ambayo yanaendelea kuwafanya wawe dhalili.
Kila mtu anatamani mambo yaache kuwa na hali ilivyo sasa, anatamani yachukue mkondo mpya na njia mbadala ambayo inaweza kuwa na matumaini. Katika hali hii unatarajia kuwa wao ndiyo wawe chemichemi na chachu ya mbadiliko.
Bahati mbaya kwetu ni kwamba, tunataka na kutamani mabadiliko lakini hatuko tayari kulipa gharama za mabadiliko hayo. Tunataka matokeo yaje tu kutoka hewani bila sisi kuhusika kwa namna yeyote ile kuyasababisha.
Katika hili tunapaswa kujifunza kwa ujumbe wa mabadiliko wa Rais wa Marekani Barack Obama kwamba “The change we seek will not come easy, that it will not come without its share of sacrifice and struggle”, kwamba mabadiliko tunayoyataka hayawezi kuja kirahisi na hayawezi kuja bila juhudi na kujitolea.
Majitoleo yanayozungimziwa hapa ni pamoja na kukubali kuachana na mazoea mabaya ambayo tunayaona kuwa kama sehemu ya maisha yetu, kwamba hata kama tunaumizwa sana na mazoea hayo, hatuko tayari kuyavua na kuvumilia uchungu kidogo wa muda ili tupate nafanikio ya muda mrefu.
Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi ambao Watanzania tunatakiwa kutumia haki yetu ya kikatiba kuchagua aina ya viongozi ambao wanaweza kutuletea mabadiliko tunayoyatamani. Tunatakiwa tuutambue ukweli kwamba mambo mazuri ya kimaendeleo tunayoyatamani yana uhusiano wa moja kwa moja na aina ya viongozi tunaowachagua.
Jiulize Mtanzania, wewe mahali ulipo una mwakilishi wako mbunge na diwani, lakini kuna kero nyingi sana mtaani kwako, katani na jimboni kwako, kiongozi huyo anatakiwa kuwa mhamasishaji wa maendeleo katika jimbo na kata yenu.
Yako mambo ambayo hayahitaji hata nguvu ya serikali kuyafanya yawezekane, mambo mengine kama barabara za jimboni kwenu, huduma za maji na vitu vya aina hiyo vinategemea sana aina ya kiongozi wenu, kama ana sifa za kufaa kuwa kiongozi anaweza kabisa kuwahamasisha ninyi wanajimbo na kata na kuishwishi serikali kuweka nguvu kidogo ili kufanikisha maendeleo yenu.
Wako Watanzania leo wana mbunge huyo huyo kwa miaka 15 au zaidi lakini hajawahi kuwa na mchango wa maana kwa katika kuhamasisha maendeleo ya jimbo lake, huyu hata kama ni mjombe wenu, mmezalia kijiji kimoja au ni swahiba wako sana, hafai kuwa mbunge wa jimbo lako.
Kama katika miaka hiyo kwa vipindi vitatu hajafanya mambo ya msingi, anaonekana jimbo mara moja kwa miezi sita, kwa mwaka anaonekana jimboni mara mbili kama sikuku za Eid el fitri na Eid al Haji, huyu hata akipewa miaka 25 mingine hawezi kuleta mabadiliko ya maana jimboni kwako.
Wabunge wa aina hii ni wajanja sana katika kipindi kama hiki anakuwa mnyenyekevu na vizawadi kwa viongozi mbali mbali wa chama na watu wenye ushawishi jimboni ili waweze kurubuni ninyi mliobaki ili mmuone ni aina ya mtu kweli mnayemhitaji.
Huyu katika hali ya kawaida anacheza na akili zenu tena ni kashfa kwenu ninyi kwa kuwa anaowaona kama watoto wadogo mnaoweza kudanganywa na ‘peremende’ mkadanganyika, na anakuwa anawapuuza hivyo hivyo kila mwaka ndiyo maana bado ni mwakilishi wenu kwa miaka yote hiyo.
Wanaharakati wa ukombozi wanamsemo mmoja kuwa “The most potent weapon of the oppressor is the mind of the oppressed”, kwamba silaha muhimu sana kwa wakandamizaji ni akili za waandamizwaji.
Ni kweli wala hatuwezi kubishana katika hili, kwamba viongozi wetu hawa wanaotuongoza wanatunyanyasa na kutumia nafasi za umma tulizowapa dhamana kutuongoza kuelekea kwenye maendeleo yetu kama taifa, wanazitumia kwa manufaa binafsi kwa sababu ya umbumbu wetu.
Mnamwona mbunge wenu yuko ‘bize’ na mambo yake kuliko ya umma ambayo aliomba kuwa mtumishi wenu ili awatumikie, badala yake hata kumona tu mmweleze maoni yenu na jinsi mnavyoona mnaweza kukabiliana na changamoto zenu katika jimbo inakuwa ni kazi ngumu kumuona kama vile unataka kuonana na malkia.
Msomaji mmoja wa Kanda ya Ziwa alieleza masikitioko yake jinsi ambavyo wamefanya juhudi za kutaka kumuona mbunge wao kwa muda wa mwaka mzima lakini hawakufanikiwa badala wanaishiakuelekezwa kuonana na katibu wake.
“Hata tulipompigia simu mara kadhaa, kwa sababu hata jimboni haishi, alituelekeza tuonane ana katibu wake tu, tukaisisitiza katibu anajua na hana msaada akasema akija atatupatia nafasi tumuone, siku amekuja kulikuwa na mafuriko ya watu hatukumuona mpaka tukakata tama, sasa ndugu mwandishi huyu kweli anafaa kuwa kiongozi?”, alihitimisha msomaji wangu kwa kunihoji.
Nilimwelewa mahangaiko aliyokuwa nayo pamoja na wananchi wenzake, lakini nilimjibu nikamwambia, katika kila jamii kuna uwezekano mkubwa wa kupata kiongozi anayewastahili zaidi kuliko mnayemtaka, kwa hiyo kumlaumu Mheshimiwa huyo inaweza kuwa ni kumonea kwa kuwa wakati wananmchagua hawakugalia sifa za mtu wanayemchagua na kuwianisha na changamoto zao ili kujua kama anaweza kuwa ni aina ya kiongozi wanayemhitaji.
Kwamba huenda walimchagua kwa kuwa ni mtu maarufu jimboni kwao, au ni tajiri sana, au ni ndugu yao, au aliwahonga sana kuliko wagombea wenzake, au alikuwa anapigiwa kampeni na watu wanaowaheshimu sana humo jimboni, nikamweleza hizo zote na zingine za kufafana nazo siyo sifa na wala hazitakaa ziwe sifa za kiongozi bora.
Na hicho ndicho huwa tunakifanya Watanzania tunapoingia katika vyumba vya kupigia kura, iwe katika uchaguzi wa kura za maoni au uchaguzi mkuu, tunatumia vigezo vya ajabu sana na kwa kweli, ashakum si matusi, ni vya kipumbavu kuchagua viongozi wetu.
Mwaka huu kama kweli ile kiu ya mabadiliko iliyopo ni ya kweli, kama sio unafiki, basi ni lazima Watanzania katika ngazi zote bila kujali kiwango cha elimu ya mtu, aina ya kazi unayofanya au mahali unapoishi, tubadilike kwanza sisi wenyewe na tuwe tayari kulipa gharama za mabadiliko.
Hivi kuna haja gani ya kuwa na mbunge kwa miaka 10 au zaidi lakini ambaye hana mchango wowote wa maana kwa maendeleo ya jimbo, naomba nieleweke ninaposema maendeleo ya jimbo, sizungumzii vijizawadi na vitakrima vinavyotolewa kwa viongozi wenu wa matawi au kata, au hata kwa baadhi ya watu maarufu, ambavyo mimi ninaviita ni vijirushwa katika ngozi ya zawadi.
Maendeleo ninayozungumzia hapa ni ya jumla na yanayofaidisha jamii nzima kama maji, barabara, elimu na huduma zingine za jamii ambazo kila mwanajimbo anaweza kujivunia kuwa hakupoteza kura yake bure.
Na kuleta mchango katika hili siyo lazima mtu awe na pesa za kutoa mfukoni, kwanza mtu mwenye kutoa pesa mfukoni kwa ajili ya maendeleo ya jimbo, huyo hafai na hana sifa za kuwa kiongozi, mchango ninaouzungumzia mimi hapa ni jinsi anavyowaunganisha wanajimbo kuweza kuzikabili changamoto zenu kwa kutumia rasilimali chache mlizonazo ili kuweza kujikwamua na hali mliyomo na kupiga hatua.
Chonde chonde Watanzania, mwaka huu ni wa ukombozi, tusipige kura kwa mazoea, tuchague aina ya mtu ambaye tunaamini anaweza kuwa msaada kwetu na siyo kwa kuwa eti ni tajiri sana, tukubali kuwa chanzo cha mabadiliko tunayoyatamani. Unapopiga yowe la Kamata mwizi! Kamata mwizi! ni sharti na wewe uwe nyuma ukimfukuza mwizi huyu kwa juhudi kubwa, ndipo wengine watakuunga Mkono.
Kadhalika mabadiliko na ukombozi wa kweli wa nchi hii unahitaji mapinduzi ya kweli, siyo ya mtutu wa bunduki wala mapanga, bali kwa sanduku la kura, ambayo lakini yatatokana na kubadilika kwa mtazamo wetu wakati wa kupiga kura.
Mungu ibariki Tanzania
drbugaywa@yahoo.com, 0754 449 421
Friday, February 19, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment