Tuesday, October 27, 2009

Karibu 2009

Karibu 2009!

Na Deus Bugaywa

Kila siku ni siku mpya, wahenga walisema, kwamba kwa mtu makini mwenye kujifunza kutokana na uzoefu na mwenye kutazama mbele leo ni siku tofauti kabisa na jana, hii ni siku nyingine inayokuja na changamoto zake. Hekima hii hata hivyo haimaanishi kwamba hakuna cha kujifunza kutokana na siku iliyokwisha.
Ni kutokana na kujifunza kutokana na makosa au mapungufu yaliyotangulia ndio maana siku inayoanza inakuwa ni mpya kwa maana kwamba yako makosa yaliyofanyika na mapungufu yalioonekana kwa hayo yakitumiwa vyema yanawez saidia leo kuondokana na makosa yale yale yaliyofanyika jana.
Kama taifa tunaanza mwaka mpya, ambao nina imani utakuwa wa kheri na neema kwa Tanzania kama tu tukijifunza kufuata kanuni ya historia kwamba ili tujue tulipo ni lazima tutazame tunakotoka, na ili tufahamu tuendeko ni muhimu sana kutazama tulikotoka na mahali tulipo sasa.
Mwaka huu utakuwa mpya kwa maana ya kuutofautisha na uliomalizika kama tu tutakubali kujifunza kutoka mwaka 2008. Mwaka wa jana umekuwa na mengi ya kujivunia lakini pia umekuwa na changamoto zake nyingi tu ambazo kama tukiamua kwa dhati, tunaweza kulikomboa taifa letu kutoka katika minyororo ya umaskini, ujinga na maradhi.
Mwaka jana umekuwa ni mwaka wa aina yake katika historia ya nchi hii, umeshuhudia kwa mara ya kwanza kuvunjwa kwa baraza la mwaziri kutokana na waziri Mkuu wa kujiuzulu kwa kashfa ya Richmond .
Katika hili liko somo moja muhimu sana kwetu kama taifa kwamba tunachokikosa hasa katika kutekeleza majukumu yetu mbali mbali ni dhamira ya dhati ya na uzalendo.
Hakuna ubishi kwamba kazi iliyofanya na kamati ya Mwakyembe na wenzake ni kielelezo na kipimo cha kujitoa kwa hali ya juu kwa kutetea hadhi na heshima ya Tanzania na Watanzania. Yako mambo mengi yanashindwa kufanyika kwa ukamilifu au hata hayafanyikki kabisa kwa sababu ya watu kutokuwa na moyo wa uzalendo kwa nchi yao .
Tumekuwa taifa la watu wa ajabu, ubinafsi umekuwa ndio mfumo wa kupigania maisha yetu, wako baadhi yetu, na ni wengi kweli, ambao hata kama akitakiwa kutimiza wajibu wake wa kawaida kabisa na anaolipwa kwa ajili hiyo hawezi mpaka kwanza ahakikishiwe kunufaika na kile anachotakiwa kukifanya.
Matokeo yake kila mtu sasa anapigana vita yake mwenyewe ili kuweza kuyafanya maisha yaende, hakuna mtu anakumbuka kwamba liko taifa ambamo ndio tunaishi na kwa vile hatuna nchini kwetu kwingine ni lazima tuhakikishe nchi yetu inakuwa salama katika hali zote.
Hakuna mtu siku hizi anahagaika na maslahi ya taifa hili, kila mtu anakufa na lwake kuhangaikia maslahi ya familia yake na vitegemezi vyake. Bahati mbaya sana ni kwamba harakati hizo za kujinufaisha binafsi zinafanyika kwa gharama ya kulibungua taifa.
Ziko dalili za wazi kabisa kwamba taifa hili sasa linajijenga taratibu lakini kwa uhakika kuwa tifa la matabaka. Hali hii nayo hakuna mtu anahangaika nayo watu wako ‘bize’ wakipigania maisha, hakuna anayekukosa usingizi kwa ajili ya mustakabali wa taifa hili.
Ubinafsi huu sasa umetufikisha katika hatua ambayo unaweza hata kusikia kinyaa kujiita binadamu. Ili kudhihirisha taifa hili na watu wake sasa wamejichoka na kushindwa kuheshimiana na kuthaminiana, tumefika hatua mbaya sana ya kipuuzi na kwa hakika ni ya kishenzi.
Kwamba sasa tumekosa ubinadamu kwa kiwango kisichoelezeka hata kufikia hatua ya kuona viungo vya binadamu mwenzako ni bidhaa ambayo unaweza kubadilishana kwa ajili ya kupata utajiri, huu ni ujuha na wendawazimu uliopindukia mipaka.
Haya yanatokea katikati ya jamii yetu na wako wanajamii ambao wanawajua kabisa wahusika lakini kwa sababu zinazojulikana na wao wenyewe tu, hawataki kujitoa kuwataja wahusika kwa ajili kulinusuru taifa hili na balaa hilo .
Kwa hiyo kama kuna somo moja tunalotakiwa tuiingie nalo kwa ajili ya utekelezaji wa maazimio ya mwaka 2009 ni kuanza kujenga uzalendo kwa ajili ya ustawi wa taifa letu. Ni lazima tutambue na kuukubali ukweli kwamba bila moyo wa kujitoa na hata wakati mwingine kuumia kwa ajili ya wengine hatuwezi kabisa kuufikia ukombozi wa taifa hili tunaoupigania.
Na kujitolea huku kunamhusu kila mwana wa taifa hili, kila anayeitwa Mtanzania na mwenye mapenzi mema na nchi hii ni lazima kwa hakika tuache kelele za kusubiri matatizo yatokee ndio tuanze kutafuta mchawi wakati mambo yalishaharibika.
Hakuna kitu kizuri ambacho unaweza kukipata ukiwa tu umetulia mahali au unasubiri wengine wakuletee, ni lazima tukubali kutimiza wajibu wetu kikamilifu. Tuaachane na utepetevu wa akili kudhani kwamba wako watu mahali fulani watakuja kutusaidia. Jinsi tunavyotaka nchi yetu iwe ni azima sisi wenyewe tuwajibike kuifaya iwe hivyo.
Rushwa na ufisadi uliotapakaa nchi hii msingi wake uko katika ubinafsi, mtumishi wa umma anafika mahali anasahau kwamba cheo hicho ni dhamana kwa hiyo anapaswa kufanya kazi manufaa ya aliyempatia dhamana hiyo.
Mwaka jana pia umetusaidia kutambua wawakilishi wetu ni watu wa aina gani, wabunge wetu ni watu muhimu na wadau wakubwa wa maendeleo ya taifa letu hasa kwa jukumu lao la kuithibiti serikali katika matumizi yake.
Uzoefu wa bunge la mwaka jana umetuonesha kwamba wakati tunaingia katika uchaguzi wa wabunge na wawakilishi wengine, yaani madiwani ni muhimu sana kuangalia aina ya mtu tunayemchagua kuliko chama. Tumeon jinsi baadhi ya wawakilishi wetu wanavyogeuka kuwa wasemaji wa serikali na wawakilishi wa vyama badala ya kuwawakilisha Watanzania wa majimbo yao .
Chama kinaweza kuwa kina sera nzuri na nzito sana za kimaendeleo lakini zikaishia katika kutamkwa tu kwenye mikutano ya kuomba kura, halafu mtu anayepewa jukumu la kuhakikisha sera hizo zinatekelezeka anakuwa hana uwezo huo.
Hili limejidhihirisha kwa uchache wa wabunge wa upinzani bungeni na baadhi ya wachache toka chama tawala, yako mambo ambayo katika hatua zake za awali yalionekna kama mchezo tu wa kuigiza kwa kupuuzwa na hata kukejeliwa na baadhi ya wawakilishi wetu lakini ambayo sasa yamegeuka kuwa masuala makubwa yenye uzito mkubwa kwa mustakabali wa nchi hii.
Kwa hiyo tunapomshukuru Mungu kutujalia kuuanza mwaka 2009 salama, tudhamirie basi kuhakikisha kwamba tunajitahid kila mmoja wetu kuweka mchago wetu chanya katika ujenzi wa Tanzania mpya ambayo kila mmoja wetu anaiotea ndoto.
Siyo bahati mbaya kwamba mimi na wewe tumebaki kuingia mwaka huu, wataalamu wa teolojia wanatuambia kwamba Mungu na makusudi maalum na kila mtu aliyemuumba, pengine kusudi lake kwako wewe Mtanzania uliyejaliwa kuwa hai mpaka wakati huu ni kuleta mabadiliko katika taifa hili.
Hakuna kinachoweza kushindikana kama tukiamua kwa dhati, kama mwaka jana tulishindwa hatuna sababu ya kulalamikia yaliyopita, kwani hayo si ndwele, sasa tugange yajayo. Na kwa kuwa kila siku ni siku mpya na hivyo mwaka huu ni mwingine tofauti na wa jana basi tuamue uwe mwaka wa ukombozi wetu katika kila uga wa jamii yetu, uwezo wa kusababisha mabadiliko tunao, kinachotakiwa ni kudhamiria tu.
Mungu ibariki Tanzania .
drbugaywa@yahoo.com 0734 449 421

No comments:

Post a Comment